
Dar es Salaam, 23 April 2025.
Hekima na Umoja;
Jumuiya ya SMAUJATA kupitia Idara ya Wanafunzi, Vyuo na Vyuo Vikuu SMAUJATA inashtushwa na kulaani vikali tukio la ukatili wa kinyama uliofanywa na wanafunzi dhidi ya mwanafunzi mwenzao, kwa kile kinachodaiwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Tukio hili ni ukiukwaji wa haki za binadamu. Ni jambo la kusikitisha sana kuona wanafunzi, ambao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa, wanajihusisha na vitendo vya kikatili kama hivi.
SMAUJATA kupitia kampeni yake ya “Kataa Ukatili, Wewe ni Shujaa” inatoa wito kwa:
- Vyombo vya dola: Kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuhakikisha wahusika wanafikishwa mahakamani na sheria iweze kuchukua mkondo wake.
- Uongozi wa Chuo: Kuchukua hatua stahiki za kinidhamu, kwa mujibu wa taratibu za chuo dhidi ya wahusika,ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hizo.
- Wanafunzi wote: Kuwa mabalozi wa amani, kutumia busara na utamaduni wa majadiliano na suluhu za amani katika migogoro ya kijamii badala ya kutumia nguvu.
- Jamii kwa ujumla: Kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola katika kupambana na ukatili wa aina yoyote ile.
- Serikali: Kuongeza nguvu katika kutoa elimu ya kujikinga na ukatili mashuleni na vyuoni, pamoja na kuweka mazingira salama kwa wanafunzi.
SMAUJATA inaamini kuwa ukatili wa aina yoyote ile haukubaliki na hauna nafasi katika jamii yetu. Tutaendelea kupaza sauti zetu kupinga ukatili na kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa waathirika.
Kataa Ukatili, Wewe ni Shujaa!
..Ushindi na Ushujaa SMAUJATA.
Imetolewa na;
Rachpa Tarimo;
MKurugenzi Mtendaji Teknolojia ya Habari na Mawasiliano SMAUJATA, HQ.