
Aprili 07,2025
Mwenyekiti wa SMAUJATA Shujaa Sospeter Bulugu, Kwa niaba ya Menejimenti ya Jumuiya ya SMAUJATA anawatakia Heri ya Kumbukizi ya Hayati Abeid Amani Karume, Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Siku hii ni muhimu sana katika historia yetu, kwani inatukumbusha juu ya uongozi wake shupavu, kujitolea kwake kwa ajili ya wanyonge, na mchango wake usioweza kusahaulika katika kuleta Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na hatimaye kuunganisha Tanganyika na Zanzibar na kuzaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Shujaa Karume alikuwa kiongozi mwenye maono, aliyeamini katika usawa, haki, na ustawi wa wote. Alisimama imara kwa ajili ya kuwakomboa wananchi na kuweka misingi ya taifa lenye umoja na mshikamano.
Tunawahimiza Wanajumuiya wa SMAUJATA na Watanzania kwa ujumla kutumia siku hii kukumbuka na kuenzi mema yote aliyotufanyia Shujaa Karume. Tuige mfano wake wa Uadilifu,Uzalendo na kujitoa kwa ajili ya maslahi ya wengi.

Siku ya Karume ni fursa ya kutafakari juu ya safari yetu ndani ya Jumuiya.Tushirikiane kwa pamoja katika kujenga Tanzania isiyo na vitendo vya ukatili na kuzidisha uwepo amani,umoja na maendeleo endelevu.
Tumuenzi Mzee Karume kwa matendo yetu mema kwa kujenga Taifa bora kwa vizazi vijavyo.
Imetolewa na Kurugenzi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano SMAUJATA, HQ