Na SMAUJATA HABARI – ARUSHA

April 14;2025
Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Kaskazini, Shujaa Ezekiel Tlanka, amefanya ziara rasmi katika Mkoa wa Arusha ambapo alipokelewa kwa heshima na Mashujaa wa SMAUJATA wa mkoa huo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Arusha. Baada ya mapokezi, walielekea katika eneo maalum lililoandaliwa kwa ajili ya kikao kifupi.
Katika kikao hicho, Katibu wa Kanda alijitambulisha rasmi kwa Mashujaa wa Mkoa wa Arusha na kuwasilisha ujumbe muhimu kutoka SMAUJATA Kanda ya Kaskazini. Ujumbe huo ulijikita katika maeneo yafuatayo:

- Usajili wa Wanachama:
Kila mwanachama anatakiwa kujisajili kwa kulipa ada ya shilingi 12,000 kwa mwaka, pamoja na shilingi 3,000 kwa ajili ya kitambulisho cha uanachama – jumla shilingi 15,000. - Kazi za Kujitolea:
Mashujaa wote wametakiwa kuendelea kufanya kazi za kujitolea ikiwemo:
Kutetea waathirika wa ukatili,
Kutoa elimu kwa wananchi,
Kuibua na kuripoti matukio ya ukatili kwa kushirikiana na vyombo vya serikali.
- Moyo wa Uzalendo:
Katibu aliwatia moyo Mashujaa akisisitiza kuwa kazi hii ni ya kujitolea bila malipo. Pamoja na changamoto kama kutokuwa na usafiri au rasilimali, kazi hii ina thawabu mbele za Mwenyezi Mungu. Alisisitiza kuwa:
“Tusivunjike moyo kwa sababu hatuna malipo. Wengine wanaweza kuona tunafanya kazi zisizo na maana, lakini tuendelee kujituma kwa kuwa Mungu anaona na atatulipa.”
- Utekelezaji wa Maagizo ya Kitaifa:
Mashujaa walihamasishwa kuendelea kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na viongozi wa SMAUJATA Taifa kwa wakati, ili kuhakikisha harakati na utendaji wa chama zinaendelea bila vikwazo.
Mwisho wa kikao, Katibu alitoa shukrani za dhati kwa Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Arusha na viongozi wote waliomsaidia kuandaa kikao hicho kwa mafanikio.
Katibu wa Kanda anaendelea na ziara yake ambapo kesho anatarajiwa kuwa katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa kikao kingine na Viongozi wa SMAUJATA wa mkoa huo.
Katika ziara hiyo, Katibu wa Kanda aliambatana na Katibu wa SMAUJATA Wilaya ya Babati, Shujaa Petro Martin.

Imetolewa na:
Idara ya Habari na Mawasiliano, SMAUJATA Wilaya ya Babati.